Jumamosi 23 Agosti 2025 - 01:51
Mjumbe wa Kambi ya Muqawama amelaani kitendo cha serikali ya Lebanon cha kukabidhi mfungwa wa Kizayuni bila kupata faida yoyote

Hawzah/ Ibrahim al-Mousawi amesema: Sisi, kama Walebanoni, tumeshangazwa na tangazo la adui Mzayuni kuhusu kukabidhiwa kwake Mzayuni mmoja na maafisa wa Kilebanoni huku makabidhiano hayo yakifaidisha upande mmoja

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Ibrahim al-Mousawi, mwanachama wa Kambi ya Uaminifu kwa Muqawama na mbunge wa Lebanon, katika tamko lake amesema: Sisi, kama Walebanoni, tumeshangazwa na tangazo la adui Mzayuni kuhusu kukabidhiwa kwake Mzayuni mmoja na maafisa wa Kilebanoni huku makabidhiano hayo yakifaidisha upande mmoja, Lebanon haikupokea hata mmoja wa wananchi wake waliokuwa katika kifungo cha adui, hili limezua maswali na shaka kubwa kuhusu uzembe na kutotumia nafasi iliyokuwepo ili kukamilisha mabadilishano na upande wa pili.

Akaongeza kwa kusema: Kile kilichofanywa na maafisa wa Kilebanoni katika uwanja huu ni jambo la kulaumiwa na la kukemewa, na kwa wananchi ni jambo la kushangaza, hili linapaswa kuwekwa mbele ya maswali na uwajibikaji wa maafisa husika, kwani linaonesha uzembe na kutowajibika kwa upande uliosimamia suala hili la kitaifa lenye umuhimu mkubwa katika mazingira haya nyeti.

Al-Mousawi akaendelea kusema: Kile kilichotokea kinaonesha wazi kabisa kushindwa kwa upande uliowajibika kutekeleza majukumu yake kwa njia ipasavyo, hasa katika jalada nyeti na muhimu kama lile la wafungwa na walioko kizuizini katika magereza ya adui.

Mjumbe wa Kambi ya Muqawama akabainisha: Hili ndilo lililowashangaza sana familia na wapendwa wao na kuwapelekea ujumbe wa aibu na kukata tamaa, kwamba serikali yao haina shauku na haijui namna ya kunufaika na nguvu zake, na inaacha bure wakati adui mporaji akiendelea kutenda jinai, mashambulizi na uvamizi wake.

Al-Mousawi akasisitiza kuwa: Maafisa husika katika mamlaka wanapaswa kubainisha kwa uwazi na kikamilifu ukweli wa kilichotokea kwa wananchi wa Lebanon, hasa familia za wafungwa, kadhalika maafisa wa kisheria na usalama husika wanapaswa kuanzisha uchunguzi wa kina ili kugundua ukweli wa kilichotokea ili hatua mwafaka ziweze kuchukuliwa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha